Home » Takwimu za Elimu

Category Archives: Takwimu za Elimu

WALIOCHAGULIWA KOZI ZA CERTIFICATE NA DIPLOMA ZA UALIMU 2017

Mwezi Juni, 2017 Wizara ilitangaza nafasi za Mafunzo ya Ualimu ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa Mwaka wa Masomo 2017/18. Tangazo lilielekeza kwamba waombaji wa programu za Ualimu katika Vyuo vya Serikali waombe kupitia tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (www.nacte.go.tz). Aidha, Wizara ilielekeza kwamba waombaji wa Udahili kwenye vyuo visivyo vya Serikali, waombe moja kwa moja vyuoni.

Baada ya vyuo visivyo vya Serikali kufanya uchaguzi vilielekezwa kuwasilisha majina ya waombaji waliochaguliwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa ajili ya uhakiki wa sifa za Udahili na kisha vyuo hivyo kutangaza waliodahiliwa. Vyuo visivyo vya Serikali vitatangaza majina ya waliochaguliwa na kuhakikiwa na NACTE kuanzia tarehe 18 Septemba, 2017.

Maombi ya Udahili kwa ajili ya Mafunzo ya Ualimu katika ngazi ya Astashahada na Stashahada katika vyuo vya Serikali yalianza rasmi tarehe 10 Juni, 2017 na kuhitimishwa tarehe 20 Agosti, 2017.

Hadi tarehe ya mwisho wa maombi,  jumla ya waombaji 15,091 (wanawake 6, 051 na wanaume 9,040) walikamilisha maombi yao. Waombaji 12,152 (sawa na 80.5%) walikuwa na sifa stahiki za kujiunga na programu za ualimu walizoziomba. Jumla ya waombaji 2,939 (19.5%) hawakuwa na sifa zinazotakiwa kujiunga na Mafunzo ya Ualimu.

Nafasi za Mafunzo ya Ualimu katika vyuo vya Ualimu vya Serikali zilizotangwa zilikuwa  ni 5,375 kwa programu ya Astashahada ya Elimu ya Ualimu na 3,731 za Stashahada mbalimbali za Elimu ya Ualimu.  Hivyo, jumla ya nafasi za Udahili kwa Mafunzo ya Ualimu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 zilikuwa 9,106 katika vyuo 30, ambapo kati yake, vyuo 23 vinatoa Mafunzo ya Ualimu katika ngazi ya Astashahada na vyuo 16 vinatoa Mafunzo hayo katika ngazi ya Stashahada.

Uchaguzi wa waombaji ulizangatia vigezo vya jumla ambavyo ni ufaulu wa wa Daraja la I hadi la III kwa  Kidato cha Nne kwa waombaji wa Astashahada na Kidato cha Sita kwa waombaji wa Stashahada. Aidha waombaji wa Astashahada waliofaulu masomo ya Sayansi katika Kidato cha Nne walipewa kipaumbele. Ufaulu wa juu kwa waombaji waliochaguliwa kwa kozi ya Astashahada ni Daraja la I, alama 14  na kwa Stashahada ni Daraja la I, alama 6.  Ufaulu wa chini  kwa waombaji wa kozi ya Astashahada ni Daraja la III, alama 25 na kwa Stashahada ni Daraja la III, alama 17.

Kozi Ufaulu wa Juu Ufaulu wa Chini
Astashahada K4: Daraja la I, alama 14 K4: Daraja la III, alama 25
Stashahada K6: Daraja la I, alama 6 K6: Daraja la III, alama 17

 

 

 

Jumla ya waombaji   7,578   wamechaguliwa na hivyo kupangiwa kwa ajili ya Mafunzo ya Ualimu katika ngazi ya  Astashahada na Stashahada katika Vyuo vya Serikali vya Ualimu. Nafasi zilizobaki wazi katika vyuo vya Ualimu vya Serikali bila kujazwa ni 1,528. Hii ni kutokana na jinsi waombaji walivyofanya  uchaguzi wa vyuo.

Majina ya waliochaguliwa yanapatikana katika tovuti za Wizara (www.moe.go.tz), NACTE (www.nacte.go.tz), na kwenye kurasa (profile) binafsi za waombaji na katika vyuo husika. Vyuo vya Ualimu vinatarajiwa kufunguliwa tarehe 25 Septemba, 2017. Aidha wale waliochaguliwa watajulishwa na vyuo husika juu ya utaratibu wa kufika na kuanza masomo.

Kwa kuzingatia kuwa bado kuna vyuo vyenye nafasi zilizo wazi, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) litatoa fursa ya kuwasilisha maombi kwenye programu za Astashahada na Stashahada katika fani mbalimbali nchini kuanzia tarehe  18 Septemba, 2017 hadi tarehe 1 Octoba, 2017.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kutoa wito kwa wahitimu wa Kidato cha Nne na cha Sita na wale wote walio na sifa za kujiunga na mafunzo mbalimbali kutumia fursa hiyo kufanya maombi ya Udahili. Waombaji wanashauriwa kufanya uchaguzi kwa umakini kwa kuzingatia ufaulu wao ili kuepuka kukosa nafasi kwa sababu ya kuchagua fani zenye ushindani mkubwa.

Taarifa hii imetolewa na katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Dr. Leonard D. Akwilapo

 

Advertisements

TAKWIMU MUHIMU ZA ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI KWA MWAKA 2016-2017

Ofisi ya Waziri mkuu, Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) imetoa takwimu mbalimbali za Elimu kwa mwaka 2016-2017 kama ifuatavyo:-

ELIMU YA MSINGI

Idadi ya wanafunzi wa shule zote za msingi kwa mwaka 2017 ni 9,317,410. Kati yao wavulana ni 4,629,027 sawa na 49.7% na wasichana ni 4,688,383 sawa na 50.3%.

Wanafunzi 8,969,110 sawa na 96.3% wanasoma shule za msingi za serikali na wanafunzi 348,300 sawa na 3.7% wanasoma shule za msingi zisizo za serikali (Binafsi).

Idadi ya walimu wa shule zote za msingi ni 197,545 kati yao walimu 179,291 sawa na 90.8% ni wa shule za msingi za serikali na walimu 18,254 sawa na 9.2% ni wa shule za msingi zisizo za serikali.

ELIMU YA SEKONDARI

Jumla ya wanafunzi 1,909,017 wanasoma elimu ya sekondari kwa mwaka 2017. miongoni mwao, wanafunzi 947,486 sawa na 49.6% ni wavulana na wanafunzi 961,531 sawa na 50.4% ni wasichana.

Wanafunzi 1,564,112 sawa na 81.9% wanasoma shule za sekondari za serikali na wanafunzi 344,905 sawa na 18.1% wanasoma shule za sekondari binafsi.

Jumla ya walimu wa shule zote za sekondari ni 110,098 kati yao walimu 89,367 sawa na 81.2% ni wa shule za sekondari za serikali na walimu 20,731 sawa na 18.8% ni wa shule za sekondari binafsi.

Kwa undani wa takwimu hizi, fungua viunganishi vifuatavyo:-

>>IDADI YA SHULE ZA MSINGI KWA KILA WILAYA, 2017

>>IDADI YA SHULE ZA SEKONDARI KWA KILA WILAYA, 2017

>>IDADI YA WANAFUNZI WA MSINGI KWA KILA WILAYA, 2017

>>IDADI YA WANAFUNZI WA SEKONDARI KWA KILA WILAYA, 2017

>>MCHANGANUO WA UMRI WA WANAFUNZI WA MSINGI KWA KILA WILAYA, 2017

>>MCHANGANUO WA UMRI WA WANAFUNZI WA SEKONDARI KWA KILA WILAYA, 2017

>>UWIANO WA MWALIMU KWA WANAFUNZI WA MSINGI KWA KILA WILAYA, 2017

>>UWIANO WA MWALIMU KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI KWA KILA WILAYA, 2017

>>FEDHA ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI KWA KILA SHULE YA MSINGI, 2016-17

>>>FEDHA ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI KWA KILA SHULE YA SEKONDARI, 2016-17

 

%d bloggers like this: