Home » Habari

Category Archives: Habari

WIZARA YATAHADHALISHA UTAPELI WA NAFASI ZA MASOMO NCHI ZA NJE

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea taarifa ya kuwepo kwa kikundi cha watu wanaojitangaza kutoa nafasi za udhamini wa masomo kwa kutumia majina ya ofisi za kibalozi. kikundi hicho kimekuwa kikiwataka waombaji kulipa ada ya maombi kiasi cha shilingi laki sita (600,000/=) za kitanzania.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutaarifu Umma kuwa Wizara haihusiki na kikundi hicho na kwamba watu hao wanafanya shughuli hizo kinyume na taratibu za Serikali. Wizara inapenda kuwajulisha watanzania wote kuwa nafasi zote za masomo zinazotangazwa na Serikali hutolewa kupitia Vyombo mbalimbali vya habari, Tovuti ya Wizara pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu. Watanzania wanaoomba kunufaika na nafasi zinazotolewa na nchi wahisani hawatakiwi kulipa malipo yoyote. Wizara inatoa wito kwa wananchi na wadau wote wa Elimu kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohuska wanapoombwa fedha kutoka kwa wahalifu hao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.

13 Oktoba, 2017

Advertisements

SHULE YAWAZAWADIA MAGARI WANAFUNZI WAKE WALIOFAULU VIZURI KITAIFA

 

Wanafunzi wawili,  Edna Meela na Byera Kaibagarauka waliohitimu kidato cha sita mwaka huu katika shule za Waja zilizopo mkoani Geita wamezawadiwa gari lenye thamani ya fedha za kitanzania shilingi 11,500,000 kila mmoja baada ya kuwemo kwenye orodha ya kumi bora kitaifa na kuipeperusha vyema bendera ya shule hizo.

Zawadi hizo zimetolewa na mkurugenzi wa shule hizo Injinia Chacha Wambura katika hafla maalumu iliyoandaliwa kuwapongeza wanafunzi hao.

Mbali na magari hayo, pia uongozi wa shule umeahidi kuwapatia petrol lita 40 kwa kila mwanafunzi kwa kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja sanjari na ofa nyingine ya kujifunza udereva ili waweze kuyatumia magari yao.

Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa wanafunzi hao (Edna Meela) mwenye miaka 21 aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa kwa kupata daraja la kwanza kwa pointi nne za masomo ya sayansi (PCM)  amesema anategemea kulitumia gari lake kwa biashara ya Uber ili limsaidie kukidhi gharama mbalimbali zikiwemo za chuo kikuu ambapo amechaguliwa kusoma chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

SAFU MPYA YA WIZARA YA ELIMU YAAHIDI USHIRIKIANO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa kitendo cha Rais John Magufuli kumbakisha kwenye Wizara hiyo ni sawa na kumchagua upya, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii.

Waziri Ndalichako amesema hayo wakati akimkaribisha Naibu waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ambaye ameapishwa leo kuitumikia Wizara hiyo.

Wakati akizungunza na Watumishi wa Wizara hiyo Naibu Waziri Ole Nasha amesema katika utumishi wake anaamini katika mambo manne ambayo ni uadilifu na uaminifu, kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ushirikiano ili kutimiza malengo ya Kitaifa.

Ole Nasha amesema hayo muda mfupi baada ya kupokelwa na watumishi wa Wizara hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kuendeleza Sekta ya Elimu.

Pichani hapo chini ni matukio mbalimbali wakati wa hafla ya kumkaribisha Naibu mpya wa Elimu William Ole Nasha

TCU YAFUNGUA FURSA KWA UDAHILI WA AWAMU YA PILI 2017/18


TAARIFA KWA UMMA
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inautangazia Umma kuwa awamu ya
kwanza ya Udahili wa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na masomo ya
shahada za awali ulimalizika tarehe 30 Agosti 2017. Tume inawaarifu kuwa
imekamilisha zoezi la uhakiki wa majina ya waombaji wote walioomba
kujiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo wa 2017/18.
Hata hivyo kutokana na waombaji wengi kutochaguliwa kutokana na sababu
mbali mbali, Tume inatangaza kuwa itafungua maombi kwa awamu ya pili
kuanzia tarehe 4 hadi 10 Octoba 2017 ili kuruhusu makundi yafuatayo kuomba
udahili:
• Waombaji watakaokuwa wamekosa nafasi kwenye awamu ya kwanza;
• Waombaji wa kidato cha Sita walioshindwa kuomba katika awamu ya
kwanza;
• Waombaji wenye vigezo vya Stashahada walioshindwa kupata Namba
ya Uhakiki wa Tuzo (AVN);
• Waombaji ambao wamemaliza mitihani ya “Cambridge” mwaka 2017
na matokeo yao yameshatoka; na
• Waliokuwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakao kuwa na uthibitsho
toka vyuo vyao vya awali.
Aidha Tume inapenda kusisitiza kuwa utaritibu wa kutuma
maombi ni ule ule uliotumika katika awamu ya kwanza ya Udahili.
Imetolewa na
Prof. Eleuther Mwageni
Kaimu Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
4 Oktoba 2017

NDALICHAKO AZINDUA BODI MPYA YA MIKOPO YA WANAFUNZI

Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezinduliwa leo Oktoba 3, 2017 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na kuitaka bodi hiyo mpya kufanyia kazi changamoto za kiutendaji na usimamizi ili kuweza kukidhi matarajio ya Watanzania.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za HESLB, Mwenge, Dar es Salaam, Mhe. Prof. Ndalichako aliwaeleza wajumbe wapya wa bodi kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa HESLB inaendelea kutoa huduma bora na ufanisi wa hali ya juu kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakurugenzi Bi. Madina M. Mwinyi. 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakurugenzi Bi. Madina M. Mwinyi akimwalikilisha Mwenyekiti, katika salamu za shukrani, amemuahidi Waziri kuwa yeye na wajumbe wote wa bodi hiyo mpya watatumia uzoefu na utaalam wao katika Sekta ya elimu ya juu ili kuboresha mahusiano na wateja wa HESLB na pia kuweka vizuri kumbukumbu za utoaji na urejeshwaji wa mikopo.

Uteuzi wa wajumbe wa bodi mpya ya wakurugenzi ulianza rasmi Agosti mosi 2017 na wajumbe hao wataisimamia HESLB kuboresha utoaji huduma kwa muda wa miaka mitatu hadi Julai 31, 2020.

Uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo unazingatia uwakilishi wa wadau mbalimbali wa elimu ya juu kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ikiwa na wajumbe 9.

Bodi mpya inajumuisha Mwenyekiti Prof. William A.L. Anangisye na wajumbe ni Bi. Madina M. Mwinyi,  Bw. Gerson Mdemu, Mhandishi Dk. Richard Masika, Prof. Caroline Nombo, Dk. Dalmas A.L. Nyaoro, Bw. Frank Nyabudege Mugeta, Bi. Suzanne Urio, na nafasi ya mjumbe mmoja kutoka Wizara ya Fedha Zanzibar ambayo itajazwa baadaye.

%d bloggers like this: