Home » 2017 » August

Monthly Archives: August 2017

WIZARA YA ELIMU: HATUJAZUIA KUSOMA DEGREE KWA WASIO NA ELIMU YA KIDATO CHA SITA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutarifu umma kuwa taarifa zinazosambaa kwa kasi  kwenye mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari

“Serikali yapiga Marufuku Kusoma Degree bila kupita Kidato cha Sita,” tarifa hiyo siyo ya kweli na haijatolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Joyce Ndalichako.

Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako hajatangaza popote na kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote.

Profesa Ndalichako yuko Mkoani Kigoma kwenye ziara ya ufuatiliaji wa Miradi ya Elimu, inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara yake.

Vile vile Wizara inapenda kutoa wito kwa watanzania kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuupotosha umma kwa taarifa ambazo siyo sahihi na  hazina ukweli wowote.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina utaratibu wake wa kutoa taarifa hivyo inawaomba radhi wale wote waliopata usumbufu kutokana na kusambaa kwa taarifa hiyo.

Imetolewa na:

Mwasu Sware

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

WIZARA YA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA

19 Agosti, 2017

VIDEO: TUKIO LA KUPATWA KWA JUA

Jana tarehe 21 Agosti, baadhi ya maeneo ya sayari ya Dunia yalishuhudia giza la mchana ikiwa ni matokeo ya kupatwa kwa jua (Mwezi kuwa katikati ya Jua na Dunia). Tukio hili ambalo hujirudia kila baada ya mwaka mmoja au miwili na kushuhudiwa na sehemu mbalimbali za dunia kwa kiwango tofauti huvuta hisia za watu wengi na pengine kuzua taharuki kwa wale ambao wanakuwa hawana taarifa au elimu ya mabadiliko hayo ya kidunia.

Elimu Leo tumefanikiwa kupata kipande cha video ya tukio la jana kama ilivyochukuliwa na shirika la safari za anga za mbali la Marekani (NASA) kikionyesha mionekano mbalimbali ya jua katika bara la Amerika ambako kwa mwaka huu ndiko tukio hilo limeonekana vizuri zaidi.

 

COREEN SWAI: BINTI WA KITANZANIA ALIYEBUNI FIMBO YA WASIOONA

Binti wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam Coreen Swai ametengeneza fimbo ya kuwasaidia kutembea walemavu wasioona. Lakini sio fimbo ya kawaida kama zile tunazozijua wengi. Hii ni ya KIPEKEE kabisa kama unavyoweza kuiona kwenye video hapo chini

Chanzo:DW

WIZARA YA ELIMU YAPOKEA VITABU VYA SAYANSI KUTOKA INDIA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepokea vitabu vya masomo ya Sayansi na Hisabati milioni moja na thelathini elfu toka serikali ya India kupitia balozi wake Saandep Arya

vitabu ambavyo vitatumika kwa wanafunzi wa kidato cha Tatu mpaka cha Sita.

Akizungumza wakati wa kupokea vitabu hivyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali ya awamu ya Tano kipaumbele chake ni kuhakikisha Elimu bora inapatikana, kwamba sayansi ndiyo kipaumbele  ili Taifa liweze kufikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa viwanda.

Profesa Ndalichako amesema kuwa Taifa la India limepiga hatua katika masula ya Teknolojia hivyo kupitia mahusuiano  mema yaliyopo kati ya nchi hizo yataifanya Tanzania kufikia malengo yake, ambapo tayari walimu hamsini wa masomo ya sayansi toka nchini India tayari wameanza kazi ya kufundisha wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.

Vitabu hivyo vinahusisha masomo ya fizikia, kemia, baiolojia na hisabati na kipaumbele kitakuwa ni kwenye shule ambazo zinamazingira magumumu katika kuzifikia.

NAFASI ZA KAZI KWA WALIMU WA MSINGI NA SEKONDARI

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

Serikali inatarajia kuajiri Walimu 92 wa Shahada na 174 wa Stashahada wa masomo ya Fizikia, Hisabati, Kilimo na Biashara kwa Shule za Sekondari na Walimu 2,767 wa Cheti kwa Shule za Msingi.

Waombaji kwa shule za Sekondari wawe waliohitimu mafunzo ya Ualimu mwaka 2016 au kabla, na wale wa Shule za Msingi wawe waliohitimu mafunzo yao mwaka 2014 au kabla.

Sifa za Waombaji:

 Walimu wa Sekondari:
(i) Shahada ya Elimu (Bachelor with Education) au Shahada ya Ualimu (Bachelor of Education) yenye somo moja la kufundishia au zaidi au Shahada isiyo ya Ualimu/Elimu yenye somo moja la kufundishia au zaidi pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu (Postgraduate Diploma in Education) kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vinavyotambulika na Serikali. Masomo ya kufundishia ni kati ya Fizikia, Hisabati, Kilimo au Biashara.
(ii) Stashahada ya Ualimu katika masomo yaliyoainishwa kwenye kipengele Na. 2.1 (i) hapo juu.

(iii) Cheti cha Kidato cha Sita
(iv) Cheti cha Kidato cha Nne

Walimu wa Shule za Msingi:
(i) Astashahada ya Ualimu iliyotolewa na Chuo kinachotambuliwa na Serikali.
(ii) Cheti cha Kidato cha Nne (wenye cheti Kidato cha Sita watapewa kipaumbele).

Utaratibu wa Kutuma Maombi:

(a) Maombi yatumwe kupitia Posta kwa njia ya Rejesta (EMS). Juu ya bahasha iandikwe kwa mkono “Maombi ya Kazi ya Ualimu – Sekondari au Maombi ya Kazi ya Ualimu – Msingi”.

(b) Mwombaji aambatishe nakala za Vyeti vilivyothibitishwa (Certified) na Mwanasheria pamoja na “Transcript”.

NB: Barua za maombi zisiwasilishwe kwa mkono. Barua zitakazowasilishwa kwa mkono hazitapokelewa.

 Masuala Mengine ya Kuzingatia:
(a) Mwombaji aandike majina yake yote matatu. Kama Vyeti vina majina mawili, utaratibu wa kisheria wa kuongeza jina uzingatiwe.
(b) Mwombaji aambatishe nakala ya Cheti cha Kuzaliwa.

Mwisho wa kupokelewa maombi ni tarehe 31/08/2017.

Maombi yatumwe kwa:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA.

Imetolewa na:

KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

%d bloggers like this: