Home » 2016 » April

Monthly Archives: April 2016

Advertisements

TAHLISO na HESLB kudumisha ushirikiano baina yao

Viongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) wamekutana mjini Dodoma kubadilishana mawazo na kukubaliana kuendeleza ushirikiano ili kutatua kero za wanafunzi.

Katika mkutano huo, uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO kutoka taasisi za elimu ya juu nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Peter Kadugalize walikutana kwa siku nzima na viongozi wa HESLB wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Jerry Sabi na kujadiliana njia bora za kutatua kero za wanafunzi wanaonufaika na mikopo.

Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Kadugalize aliiomba HESLB kuhakikisha Mameneja wa kanda wa HESLB waliopo katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya na Zanzibar wanatembelea vyuo vilivyopo katika maeneo yao na kukutana na viongzi wa Serikali za wanafunzi kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao.
Kuhusu changamoto zinazowakabili vyuoni, Bw. Kadugalize alizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wanafunzi kuhusu sifa za kupata mikopo inayotolewa na HESLB.

Akizungumzia katika mkutano huo, Bw. Sabi alisema ushirikiano kati ya HESLB na TAHLISO ni muhimu na kuahidi kuuendeleza.
Akifafanua kuhusu sifa za waombaji mikopo, Bw. Sabi alisema sifa na vigezo hutolewa kila mwaka na kuwasihi waombaji watarajiwa wa mikopo kusoma kwa makini na kuzingatia sifa hizo kabla ya kuomba mikopo.

Katika tukio lingine, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya amewataka wahitimu wa vyuo vikuu ambao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na HESLB kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu wa mwaka 2015 kutoka katika taasisi za elimu ya juu nchini waliofanya vizuri katika masomo yao iliyoandaliwa na TAHLISO, Naibu Waziri alisema watanzania wengi wanahitaji mikopo ya elimu ya juu na hivyo ni muhimu fedha hizo zikarejeshwa ili ziwanufaishe wengine.
“Kuna wengi wanaohitaji na bajeti ni finyu, ni vema mkarejesha ili ziwanufaishe wengine…na wazazi wahakikishe vijana wao waliopata elimu kwa nia ya mikopo wanaanza kurejesha,” alisema Naibu Waziri katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mt. Gaspar mjini Dodoma mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na watendaji kutoka HESLB, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), wazazi na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Jerry Sabi alisema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, jumla ya shilingi trilioni 2.3 zilikuwa zimetolewa kama mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na kuwa Bodi imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ili kurejesha mikopo iliyoiva.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji waliopata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu. Aidha, HESLB ina jukumu la kukusanya madeni yote ya mikopo ya elimu ya juu iliyotolewa na Serikali tangu mwaka1994/1995.

Advertisements

Ada elekezi: Serikali imefikia hatua hii

images

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, mhandisi Stella Manyanya.

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, imeanza zoezi la kupanga shule katika makundi ili kuweka viwango vya ada kwa kuzingatia ubora wa huduma na kwamba haitaathiri ubora wa elimu.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya, aliyasema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema). Mdee alitaka kufahamu iwapo Serikali imebaini kiwango cha gharama kwa kila mwanafunzi kwa shule za bweni na kutwa, iwapo hakitasababisha kuporomoka kwa ubora wa elimu.

Manyanya alisema wizara hiyo imefanya utafiti kuhusu gharama za kila mwanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari.

“Baada ya utafiti, wizara yangu ilifanya mazungumzo na baadhi ya taasisi zinazosimamia elimu kwa shule zisizokuwa za Serikali na kukubaliana jinsi ya kufikia viwango vya ada elekezi,” alisema.

Alisema wizara inatarajia ubora wa ada elekezi hautaathiri elimu kwa shule binafsi, kwa sababu itapangwa kulingana na ubora wa miundombinu ya shule.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) alitaka kufahamu jinsi Serikali inavyotaka kupanga bei elekezi wakati imeifanya elimu kuwa biashara.

Manyanya alisema siyo mara ya kwanza kwa Serikali kupanga bei elekezi kwa faida ya wananchi na kwamba, imefanyika kwa upande wa huduma ya maji hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura) wamefanya.

“Mwekezaji awe na fedha ya mitaji na si kutumia fedha zinazotokana na ada ya wanafunzi,”alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alihoji ni lini serikali itakaa na wadau wa elimu baada ya serikali kufanya utafiti na wamiliki nao kufanya utafiti wao?

Akijibu swali hilo, Manyanya alisema gharama za shule zitapangwa kulingana na madaraja na hivyo kutoa bei halisi itakayochochea uwekezaji uliohalisi.

Chanzo: Mwananchi

Hii imetufikia kutoka Mzumbe University, wanafunzi waaswa kufanya mabadiliko

705382_334949699945496_1855791943_o

TANGAZO MUHIMU KWA WANAFUNZI WOTE

HESLB yaingia mkataba na kampuni ya CreditInfo kuratibu taarifa za wadaiwa wote mikopo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi (kushoto) na Bw. Davith Kahwa, Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd wakibadilishana nakala za mkataba. Wengine ni Bw. Robert Kibona na Bw. Frimat Tarimo kutoka HESLB na Bw. Van Reynders, Meneja wa CreditInfo Tanzania. (Picha: HESLB)

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwishoni mwa wiki imesaini mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kufikishwa katika Kitengo Uratibu za Taarifa za Mikopo (Credit Reference Bureau) kilichopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

  
Kampuni ya CreditInfo Ltd ina leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Hivyo basi, mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambaye ataomba mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya kifedha hapa nchini, taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji huyo ni munufaika wa mkopo wa elimu ya juu na ikiwa ana nidhamu ya kurejesha mikopo.

Kwa mujibu wa mkataba huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kampuni ya CreditInfo ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji zinapatikana kwa taasisi zote za kifedha, yakiwemo mabenki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa mikopo mipya kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“HESLB ina furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya kukopesheka na taasisi za kifedha,” amesema kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd Bw. Davith Kahwa amesema lengo la kampuni yake ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinazongezeka na wakopaji wanakuwa na nidhamu kwa mikopo waliyopata.
  
“Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao wamekuwa wakilipa watapata fursa ya kipekee ya kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu wanayoionyesha kwa mikopo yao,” amesema Bw. Kahwa katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Meneja wa CreditInfo Tanzania Bw. Van Reynders.

”Tumedhamiria kuiunga mkopo HESLB katika kutekeleza majukumu yake hususan yale ya ukusanyaji mikopo iliyoiva,” ameongeza Mtendaji Mkuu huyo wa CreditInfo Tanzania Ltd. 
HESLB ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005 ili kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali tangu mwaka 1994.

Hadi sasa, zaidi ya Tshs 2.1 trilioni zimetolewa kwa watanzania na, kati ya hizo, Tshs 258 bilioni zimeiva na hivyo kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika. Kiasi kilichobaki kinajumuisha fedha walizopewa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo na ambao muda wa kuanza kuwadai (miezi 12 baada ya kumaliza masomo) haujafika.

CreditInfo Tanzania Ltd ni sehemu ya Kampuni ya Kimataifa inayofanya kazi kwenye nchi zaidi ya 20 duniai na inayojishughulisha na usimamizi wa taarifa za mikopo. Ilisajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2013.
%d bloggers like this: